Tatizo hili pia huitwa ‘false Pregnancy’ au Phantom Pregnancy au Hysterical Pregnancy’ na wataalamu wengine huita ‘Pseudo pregnancy’.Mwanamke mwenye tatizo hili hujihisi ni mjamzito lakini baada ya muda huona siku zake kama kawaida.
Mwanamke anakuwa na dalili zote za ujauzito   kama matiti kujaa, chuchu kuuma, kuhisi kichefuchefu na hata kutapika asubuhi au kutopenda baadhi ya vyakula lakini baada ya mwezi mmoja yaani tarehe zake zinapofikia anaziona au anapitiliza wiki moja au siku kadhaa.Wengine wakipima mkojo wa mimba huonyesha wana ujauzito lakini kumbe hawana mimba.
Nani anapatwa na hali hii?
Kwa ujumla hali hii inakera na kumkosesha raha mwanamke na mwenzi wake endapo walikuwa wanasubiria kwa hamu ujauzito huo. Wanaoathirika zaidi na tatizo hili ni wale wanaotafuta mimba kwa muda mrefu au wale wanaoogopa kupata ujauzito kwamba hawapo tayari kwa kipindi hicho kutokana na shughuli walizokuwa nazo kwa kipindi hicho au bado wanalea.
Chanzo cha tatizo
Tatizo hili kwa ujumla ni la kisaikolojia ambapo aidha mwanamke ana hamu sana na kupata ujauzito au anaogopa kupata ujauzito kwa kipindi hicho. Hali hii ya kisaikolojia huathiri mfumo wa homoni wa mwanamke kwa kiasi kikubwa.
Katika hali hii ya mabadiliko ya mfumo wa homoni, hata mwenendo wa mwili hubadilika na kuonyesha dalili za wazi za ujauzito.Wapo wanaume ambao hupata dalili za ujauzito wake zao wanapokuwa wajawazito, hili pia tutakuja kuliona katika makala zijazo.
Dalili za tatizo
Tatizo hili humuathiri zaidi mwanamke anayetafuta mtoto kwani homoni za ujauzito huwa juu wakati hana ujauzito hivyo kuzuia mayai kupevuka na hivyo hapati ujauzito.
Dalili za tatizo linafanana sana na dalili za kawaida za ujauzito wa ukweli na ni vigumu kutofautisha kwani wakati mwingine hata tumbo la mama huonekana kubwa na mama atakuambia anahisi mtoto anacheza na wengine huanza hata kliniki lakini ndani hakuna mimba.Dalili kuu zinazojitokeza hapa ni kufunga hedhi,  kutapika asubuhi, matiti kuuma na uzito wa mwili kuongezeka.
Wapo wengine tumbo hukua kila mwezi na huwa mjamzito kabisa hata muuguzi anaweza kuamini kuwa ni mjamzito lakini akipapasa tumbo hakuna mtoto.Kitaalamu chanzo halisi cha tatizo hili ni kuwepo na msongo wa mawazo juu ya kupata ujauzito, kama unautafuta au hauhitaji hivyo mfumo wa homoni katika ubongo hubadilika na kusababisha baadhi ya homoni za ujauzito kutoka, mama kupata tatizo la kufunga choo, uzito kuongezeka na kuongezeka kwa mwenendo wa gesi tumboni.
Wanawake wengi wanaopata tatizo hili ni wale walio kwenye ndoa au uhusiano wa kutafuta mtoto na hawajawahi kupata ujauzito. Wengine ni wale ambao tayari wameshazaa mara moja bila tatizo sasa wanatafuta ujauzito wa pili unakuwa mgumu au wangependa kubadilisha jinsia.
UCHUNGUZI
Uchunguzi wa tatizo hili hufanyika kwa madaktari wa magonjwa ya kinamama ambapo vipimo mbalimbali hufanyika na ushauri wa kisaikolojia utatolewa. Vipimo vya Ultrasound na homoni vitafanyika na kuthibitisha tatizo na kuona ukubwa wake. Kabla ya hapo historia makini ya tatizo itachukuliwa.
Tatizo hili huweza kuambatana na ugumba hivyo itabidi kuangalia uwezo wa mwanamke kubeba mimba na uwezo wa mwanaume kumpa mwanamke mimba kwani siyo kila mwanamke anayepata damu ya hedhi anaweza kupata mimba na siyo kila mwanaume mwenye uwezo wa kufanya tendo la ndoa kikamilifu ana uwezo wa kumpa mwanamke mimba.
Katika uchunguzi wa tatizo hili itazingatiwa hali halisi ya uzazi kwa wote, yaani mwanaume atapimwa mbegu za kiume na mwanamke atapimwa homoni, kizazi na mirija yake, ndipo tiba itatolewa.
USHAURI
Endapo utakumbwa na tatizo hili, basi usiwe na mawazo mgando kudhani una ujauzito wakati huna.  Pamoja na kupima mkojo wa mimba lakini pia ni vyema kuhakikisha vipimo vingine kama Ultrasound na daktari akupime kwa mikono kuhakikisha uwepo wa mtoto.

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget