Bondia
Francis Cheka akiongea na wanahabari baada ya kumchakaza Thomas Mashali
tarehe 1 Mei, 2013 katika ukumbi wa PTA jijini Dar Es Salaam.(Picha na
Maktaba)
BONDIA maarufu nchini wa
ngumi za kulipwa, Francis Cheka amehukumiwa kifungo cha miaka 3 jela na
kutakiwa kulipa fidia ya Sh. millioni 1 kwa kosa la kumpiga na kumjeruhi
meneja wa baa yake (Cheka) iitwayo Vijana Social iliyopo Morogoro
Mjini.
Akimsomea mashitaka, Hakimu wa Mahakama ya
Mkoa wa Morogoro, Said Msuya alisema Cheka alikutwa na hatia ya kumpiga
aliyekuwa meneja wa baa yake aitwaye Bahati Kabanda 'Masika'.
Alisema kuwa Cheka alitenda kosa hilo Julai
2, mwaka jana ambapo meneja huyo alikwenda kwenye baa hiyo kudai fedha
zake alizokuwa hajalipwa na bondia huyo wakati akifanya kazi ya umeneja
katika baa yake hiyo.
Hakimu Msuya alisema kuwa Cheka alikataa kumlipa na kumshushia kipigo kilichosababisha kulazwa hospitalini.
Baada ya hukumu hiyo huku Cheka
akipandishwa kwenye difenda tayari kupelekwa gerezani akionekana
kutokuwa na wasiwasi wowote, mashabiki wake walimvaa meneja huyo
wakitaka kumshushia kipigo hivyo kuibua taharuki mahakamani hapo.
Hata hivyo, baadhi ya mashabiki hao
walikuwa wakisema wapo tayari kujichanga ili kukata rufaa wakiamini kuwa
bondia huyo ameonewa.
Mbali na hukumu hiyo mahakamani hapo,
kulikuwa na kesi nyingine mbili zilizokusanya umati, moja ikiwa ni ya
Sheikh Ponda juu ya uchochezi na ile ya mtoto wa boksi inayowakabili
baba na mama Nasra.