KWAKO
mtaalamu wa Hip Hop uliyeibeba Ilala nzima begani, Rashid Makwilo ‘Chid
Benz’, mambo vipi mzazi mwenyewe? Uko poa? Mishe zinasemaje?
Ukitaka kujua hali yangu, mimi niko poa na ninaendelea na majukumu
yangu ya kujenga taifa kama kawaida na barua hii ni sehemu ya majukumu
yangu ya kazi hivyo lazima nikuandikie tu, sina jinsi.
Dhumuni la
barua hii kwanza kabisa ni kutaka kukukumbusha kidogo umuhimu wako
katika jamii. Sitaki kuamini kwamba hujui umuhimu wako lakini
kukumbushana ni muhimu, binadamu tumeumbwa kusahau.
Chid wewe ni mwakilishi mzuri sana wa Muziki wa Hip Hop. Tangu
kipindi kile ulichosumbua na wimbo wako wa Dar es Salam Stand Up na
nyingine kibao.Ulikuwa hukosei, ulikuwa unaachia jiwe baada ya jiwe na
kila mtu alikuwa anakubali uwezo wako.
Kudhihirisha wewe ni mkali, nakumbuka ulikuwa ni lulu katika suala
zima la kolabo. Wasanii walikuwa wakipanga msururu kukusaka, waliamini
ukiingiza sauti yako katika nyimbo zao basi nazo zitakuwa tamu kama
mcharo.
Hilo halikuwa na kificho, ulifanya kolabo nyingi sana. Nyimbo kama
Neila ya Tunda Man, Hao na nyingine kibao zilinoga sana pale ulipoingiza
sauti yako yenye mamlaka ambayo ulijua kuipangilia na kuendana na biti,
wewe ni mkali aisee!
Pamoja na uzuri huo, juzikati hapa liliingia suala la wewe kunaswa na
madawa ya kulevya. Binafsi sikushtuka sababu dalili za wewe kutumia
nilishaziona kabla.Niliona dalili kutokana na matendo yako, yalikuwa
hayafanani na uwezo wako mkubwa wa kutunga mashairi yenye uzito. Matukio
kama yale ya kumdunda msanii mwenzako, Rehema Chalamila ‘Ray C’,
nilijua kabisa si wewe.
Lilipokuja kutokea lile la kukamatwa na madawa pale Air Port,
nilisikitika sana kama shabiki wako. Suala la wewe kuanza kuingizwa
kwenye mikono ya sheria ni kuzidi kudidimiza kipaji chako na muziki wako
kwa jumla.
Nilifuatilia kwa makini kesi yako hadi pale ulipotakiwa kulipa faini
nikasema ni jambo la heri lakini unapaswa sasa kubadilika kweli na
kutokubali kurudi nyuma. Uliwahi kukiri kuwa unatumia madawa, ukaahidi
kuacha lakini ukarudia.
Nikushauri, mimi pamoja na mashabiki wengi Bongo na nje tunakupenda
na tunahitaji kuendelea kusikia ‘madini’ yako.Ngoma yako ya Kimbiza
ambayo haina muda mrefu sana tangu uiachie inatosha kuonesha kwamba
uwezo unao, tupe raha kama ile ambayo ulikuwa unatupa.
Achana kabisa na madawa ya kulevya, sitegemei kukuona tena unakamatwa
au unahusishwa katika suala hilo kwa namna yoyote.Ni matumaini yangu
utabadilika kweli, kwa leo ni hayo, kila la kheri!