Wapenzi wa burudani ya muziki wa kizazi kipya na muziki wa taarabu
watapata burudani ya funga mwaka kutoka kwa gwiji wa muziki wa kizazi
kipya ambaye anatamba kwa vipao mbalimbali vipya Diamond Platnumz na
mfalme wa muziki wa taarabu Mzee Yusuf na kundi lake la Jahazi Modern
Taarab watapanda jukwaa moja katika”Tamasha la Wafalme”litakalofanyika
katika ukumbi wa Dar Live,Mbagala jijini Dar es Salaam.
Tamasha hili la wafalme ambalo limeanza kuwa gumzo la jiji kutokana
na kuwa na burudani za aina mbalimbali kwa ajili ya kukonga nyoyo za
wapenzi wa burudani limedhaminiwa na kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom
Tanzania.
Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania Matina Nkurlu amesema
kuwa Vodacom imeamua kudhamini tamasha hili kwa ajili ya kuwapatia
furaha na burudani wateja wake na wananchi kwa ujumla katika msimu huu
wa sikukuu ya Krismas na mwaka mpya.
“Kama ilivyo kauli mbiu yetu kuwa“ukiwa na Vodacom maisha ni
murua”tunahakikisha mbali na kutoa huduma bora kwa wateja wetu pia
tunajua kuwa kuna muda wanahitaji kufurahi kwa burudani hivyo ndio
maana tunadhamini matamasha ya aina hii na tutaendelea kufanya hivyo
siku zote ikiwa ni moja ya njia ya kusema ahsante kwa wateja wetu kwa
kutuunga mkono”Alisema.
Mbali na tamasha la wafalme, Nkurlu alisema kampuni hiyo imeandaa
matamasha makubwa ya burudani ya wazi yatakayofanyika katika ufukwe wa
bahari Coco Beach moja litafanyika Desemba 26 na lingine litafanyika
siku ya mwaka mpya ambapo wanamuziki wanaotamba nchini watashiriki
kutoa burudani.
Naye Mratibu wa Tamasha la Wafalme Abdalah Mrisho amesema kuwa
wapenzi wa muziki wategemee kupata burudani ya funga mwaka ambayo
itaacha historia katika mwaka huu kwani imeandaliwa katika hadhi ya
kimataifa.Alisema katika kuhakikisha wananchi wanapata burudani ya
kutosha tamasha litaanza saa tano asubuhi mpaka saa tisa usiku na
kiingilio kitakuwa shilingi elfu kumi na kwa wale watakaopenda tiketi za
VIP ni 20,000.