Stori Na Musa Mateja/Ijumaa Wikienda
BAADA ya kukiri kwa mdomo wake kutumia madawa ya kulevya ‘unga’ na
baadaye ‘kustaafu’, madawa hayohayo yamemletea msanii Rehema Chalamila
‘Ray C’ ‘msala’ ambao umemfanya yeye mwenyewe, kwa hiari yake, bila
kusukumwa ajisalimishe polisi.
Msanii wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ akiwa Hospitali ya Mwananyamala .
Hivi karibuni, Ray C alijikuta akiangua kilio ndani ya Kituo cha
Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’, Dar baada ya kuhusishwa na ishu ya
uuzaji wa unga.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Ray C au Kiuno Bila Mfupa alidai
alishtukiwa na mtu wa intelejensia (usalama wa taifa) ambaye amekuwa
akimfuatilia kutoka nyumbani kwake Mbezi Beach, Dar anakoishi kwa sasa.
KAWE DARAJANI
Chanzo hicho kilinyetisha gazeti la Ijumaa Wikienda kwamba, siku ya
tukio, wakati Ray C akitokea nyumbani kwake, alipofika maeneo ya Kawe
Darajani aliona pikipiki ikimfukuzia na baadaye ikampita na ‘kumbloku’
kwa mbele.
Ilisemekana kwamba baada ya kusimama, jamaa alishuka kwenye pikipiki
kisha akamwambia aegeshe pembeni gari lake aina ya Toyota Carina TI.
Ray C katika pozi.
Chanzo kilidai kwamba, Ray C alikataa kufanya hivyo kwa kuhisi aliyekuwa akimwamrisha ni jambazi.
Ray C alimua kuondoa gari kwa kulazimisha ambapo alimkwepa jamaa huyo kisha kukanyaga mafuta ambapo gari liliondoka kwa kasi.
LUGALO Ilisemekana kwamba baada ya kufika kwenye
kituo cha daladala cha Lugalo alisimama na jamaa huyo aliyekuwa
akimfukuzia akaegesha pikipiki mbele yake na kumtaka Ray C ashuke ndani
ya gari kwani alitaka kulipekua akimwambia kuwa alikuwa amebeba unga.
Ishu hiyo ilizidi kumtia Ray C wasiwasi na kumuuliza jamaa huyo ni nani ambapo alitoa kitambulisha kuwa yeye ni askari.
Kwa kuwa hakuwa na sare, Ray C hakuamini jambo lililosababisha jamaa huyo kumuonesha kitambulisho kilichokuwa kimechakaa.
‘Ray C’akiingia kwenye gari lake aina ya 'Toyota Carina'.
MAELEWANO YASHINDIKANA
Baada ya kuona hivyo, Ray C alimwambia waongozane hadi Kituo cha
Polisi cha Oysterbay lakini jamaa huyo alikataa na kumtaka waende Kawe
jambo ambalo Ray C alishindwa kuafikiana nalo na kuondoa gari lake
akimwambia waambatane hadi kituo kidogo cha Polisi cha Mwenge.
Jamaa huyo alionekana kutotaka kwenda hivyo Ray C aliondoa gari kwa
kasi na kuelekea Mwenge ambako alikuwa akiomba msaada kwa matrafiki na
alipoona wanachelewa aliondoa gari kumkimbia jamaa huyo.
Ilisemekana kwamba awali alitaka kukimbilia Kituo cha Polisi cha
Mwenge lakini alipoona kuna msongamano alikimbia kwenda kujisalimisha
Mabatini huku akiangua kilio.
Taarifa zilidai kwamba jamaa huyo aliendelea kumfukuzia Ray C hadi
Mabatini ambapo yeye alibana nje wakati Ray C akiwa kwa mkuu wa kituo.
Hata hivyo, baadaye jamaa huyo naye alijisalimisha kwa mkuu wa kituo
ambapo naye alijieleza kwamba aliambiwa na watu wa usalama kuwa
afuatilie gari hilo lililohisiwa kubeba unga.
Ilielezwa kwamba mkuu huyo wa kituo ameamuru jamaa huyo kuchunguzwa ili kubaini malalamiko ya Ray C.
Mwanadada kiuno bila mfupa 'Ray C'.
BOFYA HAPA KUMSIKIA RAY C
Baada ya kushibishwa taarifa hiyo,
Ijumaa Wikienda lilimtafuta Ray C ambaye alielezea mkasa mzima.
Alifunguka: “Ni kweli ulivyoambiwa tulitoka Lugalo na kuelekea Mwenge
baada ya kufika kwenye Makutano ya Mwenge niliwaona askari wawili na
trafiki akiwa pembeni nikawasimamisha na kuwaeleza.
“Askari mmoja alikubali kupanda kwenye gari langu nikaenda naye hadi Mabatini.
“Baada ya kufika Mabatini nilieleza kila kitu kwa mkuu wa kituo hivyo akaniambia nisiwe na wasiwasi.
“Baada ya hapo mkuu wa kituo aliita askari wa kike na wa kiume
nikaongozana nao hadi katika gari langu na kupekuwa kila sehemu lakini
wakasema hapakuwa na chochote kibaya, hivyo nikawa nalia tu na mkuu wa
kituo akaniomba ninyamaze na kuniruhusu nikaondoka zangu kwenda
Mwananyamala hospitali kumeza dawa.
“Kama kweli alikuwa ni mtu wa usalama au askari, alitakiwa kuvaa sare
na kufuata utaratibu wa kunipekua na siyo kunikimbiza kwani nilijua ni
jambazi.
“Nusura nife kwa presha kwani nilijua ni mtu mbaya tu anataka
kunidhuru afya yangu, lakini namshukuru Mungu sikupaniki zaidi ya kulia.
Hata hivyo mkuu wa kituo ameahidi kulishughulikia suala hilo kwa
kufanya uchunguzi baada ya jamaa huyo naye kujisalimisha polisi.”